Serikali Kushirikisha
Wataalamu Kuikwamua Sekta ya Utalii, Ukarimu
Na Vincent Mpepo-OUT
Serikali imesema kuwa itaendelea
kushirikisha wataalamu na watafiti katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto
zinazoikabili sekta ya Utalii na Ukarimu ili kuibua fursa na bidhaa mpya
kupitia sekta hiyo kwa lengo la kuongeza pato la taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Meja
Jenerali Gaugence Milanzi, Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii wakati
akifunga wa Kongamano la Kimataifa la Utalii, Ukarimu na Ubunifu kwa Nchi zinazoendelea jijini Dar es salaam
lililoandaliwa na Idara ya Utalii na Ukarimu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Alisema kuwa kongamano hilo
limekuwa mwanzo mzuri wa kuwakutanisha wataalamu, watafiti na wadau wa ndani na
nje ya nchi ambao kwa pamoja wamejadili changamoto zinazoikabili sekta ya
utalii na ukarimu na kushirikishana uzoefu katika kupata suluhisho.
“Kongamano hili liwe mwanzo mzuri
wa kuendelea na mijadala mingine kwa siku zijazo kwa lengo la kupata mawazo
yatayosaidia kukuza sekta ya utalii”,alisema Meja Jenerali Gaugence Milanzi.
Alisema serikali kwa upande wake
itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuwa ni kivutio kimojawapo kwa
wageni na watalii hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuendelea
kuwa wakarimu kwa watalii na wageni.
Aidha aliwaasa wananchi kutokuwa
na mawazo hasi kwa sheria ya ongezeko la kodi (VAT) katikalinaloigusa sekta ya
utalii na ukarimu kwani ina malengo mazuri ya kuongeza mapato ya serikali
ambayo yatatumika katika uboreshaji wa huduma za jamii na miundombinu.
“Tujipe muda wa kuona matokeo ya
utekelezaji wa sheria hii badala ya kuwa na mawazo hasi kwa sheria hiyo”
Kwa upande wao, waandaji na
washiriki wa kongamano hilo wameishauri serikali kuwatumia wataalamu na
watafiti hapa nchini katika sekta ya utalii na ukarumu ili mchango wao usaidie
kuboresha sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.
Akiwasilisha majumisho ya
kongamano hilo, Daktari Shogo Mlozi, Mhadhiri na Mkuu Idara ya Utalii na
Ukarimu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alisema kuwa serikali iwatumie
wataalamu na watafiti kutoka hapa nchini katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto
katika sekta ya utalii na ukarimu.
“Ni muhimu serikali ikahusisha
wataalamu katika uundaji wa sera na miongozo mbalimbali kwani watatoa utalaamu
wao kwa manufaa ya Taifa”, alisema Dkt. Mlozi.
Alisema kuwa watafiti na
wanataluuma wana nafasi kubwa ya kutoa mchango katika uboreshaji sekta ya
utalii kupitia tafiti ambazo zikizingatiwa zinaweza kusaidia katika uboreshaji
wa sekta ya utalii hivyo kuiimarisha sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitivo
cha Sanaa na Sayansi ya Jamii, Dkt.Felician Mutasa alisema kuwa kuna hazina
kubwa ya wataalamu ambao wakishirikishwa wanaweza kutoa mchango katika sekta ya
utalii kupitia tafiti, ushauri na uboreshaji wa sera ya utalii kwa manufaa ya
nchi.
Profesa Elifas Bisanda, Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alisema kuwa bado kuna changamoto nyingi
katika sekta ya utalii lakini zaidi katika ukarimu amabapo watanzania
hawajajidhatiti katika utoaji huduma bora kwa watalii na wageni.
Akitolea mfano changamoto wa
huduma za hoteli hasa kwa upande wa chakula alisema kuwa si ajabu mgeni anaweza
kuambiwa asubiri kwa muda fulani na hatimaye akaambiwa chakula bado hata baada
ya muda huo kupita swala linaloitia doa sekta hii ukilinganisha na huduma
katika hizohizo katika nchi nyingine.
“Jambo la msingi ni kujitathimini
ni kwa namna gani tunawajali wageni na watalii katika utoaji wa huduma”,alisema
Profesa Bisanda.
Alisema kuwa kuna umuhimu wa
jamii kuelimishwa ili ijue namna ya kuwahudumia na zaidi kuwajali wageni na
watalii ili kuwafanya wapende kuja Tanzania na wawe mabalozi wazuri wakirudi
nchini kwao.
Kwa miaka ya hivi karibuni
takwimu zinaonesha kuwa sekta ya utalii imetoa mchango mkubwa katika pato la
taifa wa hadi aslimia zaidi ya 17 na asilimia 25 ya fedha za nje hivyo ni
muhuimu serikali ikaipa kipaumbele.
Kongamano hilo la kimataifa katika Utalii na Ukarimu
liliandaliwa na Idara ya Utalii na Ukarimu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ikewemo Shirika la Hifadhi la Taifa, Serena
Hotels, Leopard Tours Limited, Hyatt Regency na Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha na Kituo cha Mikutano cha Mwlalimu Julius Nyerere.
No comments:
Post a Comment