Serikali
yashauriwa kuboresha sera ya uchumi
Na Vincent Mpepo-OUT
Serikali imeshauriwa
kuboresha sera na mifumo ya uchumi wa viwanda ambayo itasaidia kuleta maendeleo
ya haraka katika kukabiliana na umasikini na kuboresha hali za maisha ya
watanzania hivyo kukuza uchumi wa nchi na pato la mtu mmoja mmoja.
Ushauri huo ulitolewa
na wahiriki wa warsha ya Sera za Viwanda, Mifumo ya Uchumi na Mabadiliko ya Kimaendeo iliyofanyika mwishoni
mwa wiki katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es Salaam.
Mtoa mada katika warsha
hiyo, Dk Piergiuseppe Fortunato alisema
kuwa nchi za Afrika zinatakiwa kutunga sera mathubuti za uchumi wa viwanda zitakazosaidia kutatua changamoto za umaskini,
ukosefu wa ajira na teknolojia duni.
“Maendeleo ya kiuchumi katika nchi yoyote
yanaenda sanjali na uwepo wa sera na mifumo madhubuti ya itakayosimamia
matumizi bora ya rasirimali na kutatua
changamoto zinazoikabili nchi,”
alisema Dk Fortunato.
Alisema serikali za
nchi za Afrika zinahitaji sera ambazo zitagusa sekta maalumu kwa nchi husika na mifumo ya uzalishaji katika
sekta hizo ili kuzipa msukumo utakaoleta matokeo mazuri na tija katika ukuaji
wa uchumi wa nchi.
Akichangia mada katika
warsha hiyo, Sylivatus Kashaga kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi alisema
kuwa warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa imemsaidia kujifunza uzoefu kutoka nchi
zilizofanya vizuri kwa mfano Vietnam ambayo uchumi wake kwa sasa umeimarika.
“Kwa kuangalia takwimu inaonesha kuwa
Tanzania na Vietnam tulianza pamoja kwa kuwa malengo ya kilimo na mazingira
yanafanana likini wao wamepiga hatua zaidi ndio maana kuna wakati tumekuwa
tunaagiza mchele kutoka Vietnam,”alisema Kashaga.
Aliongeza kuwa bado
kuna nafasi ya Tanzania kufanya vizuri katika uchumi kwa kuwekeza katika kilimo
na uzalishaji wa mazao ya biashara kwa kuyaongezea thamani hivyo kukuza masoko
ya kitaifa na kimaifa.
Dk Deusdedit Rwehumbiza
kutoka Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa warsha
hiyo imesaidia washiriki kujadili na kuainisha maeneo katika uzalishaji wa viwanda
ambayo yanaweza kuikomboa nchi kiuchumi iwapo yatapewa kipaumbele.
Pia alisema,” warsha
hiyo imekuja wakati muafaka wakati Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika
juhudi za kufufua na kuanzisha viwanda vipya kama mkakati wenye lengo la
kuimboa nchi kiuchumi”.
Kwa upande wake, Akinyi
Sassi, Mhadhiri Msaidizi katika Kitivo cha Uongozi wa Biashara-Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania alisema kuwa warsha hiyo imewasaidia kuwakumbusha washiriki
matumizi mazuri ya rasilimali za nchi kwa kuangalia manufaa ya muda mrefu
kuliko ya muda mfupi.
Akitolea mfano ugunduzi
wa gesi Sassi alisema kuwa ni vizuri kwa nchi kujenga uwezo kwa Watanzania
kuvuna na kuzitumia maliasili za nchi kwa manufaa yao kuliko kuwa na
uwekekezaji ambao utadumu kwa muda mfupi na kufifia hapo baadaye.
“Tunakaribisha wawekezaji kutoka nje,
lakini tunatakiwa kuhakikisha kuwa Watanzania wanawekeza kwenye maeneo mengine,
ili ikitotokea maliasili zetu zinapungua au kwisha tunabaki kwenye uchumi imara,” alisema.
Naibu Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Taaluma), Profesa Muganda alisema kuwa washiriki
watumie mafunzo na mijadala katika warsha hiyo kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao na
kuwaasa watunga sera kuchukua masuala muhimu yaliyojadiliwa na kuyafanyia kazi.
Warsha hiyo ya siku
tatu iliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa lijulikanalo kama UNICTAD
linaloshughulikia masuala ya biashara na maendeleo ya uchumi kwa kushirikiana
na Kitivo cha Uongozi wa Biashara-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kuhudhuriwa
na washiriki mbalimbali kutoka katika Taasisi za Elimu ya Juu, watunga sera na wawalikishi
kutoka wizara mbalimbali.
No comments:
Post a Comment