Saturday 22 October 2016



OUT yamkumbuka Mwl Nyerere kwa Muhadhara 

Na Vincent Mpepo-OUT

Katika kuadhimisha miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeadhimisha kwa kufanya muhadhara wa wazi ambao umeshirikisha wanazuoni katika fani mbalimbali chuoni hapo na mada kuu iliwasilishwa kama sehemu ya kukumbuka na kuenzi mchango wa muasisi huyo kwa  Taifa.

Akiwasilisha mada katika mhadhara huo, Mhadhiri Mwandamizi Dkt Neville Reuben alisema kuwa Mwl Nyerere alikuwa na maono ambayo kama yangeendelezwa kiutekelezaji yangesaidia kulifikisha taifa hili mbali katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwani alisisitiza katika elimu.

“Mwl Nyerere aliamini kuwa elimu ndiyo nyenzo kuu ya kuondoa ujinga, umaskini na maradhi”, alisema Dkt. Reuben

Alisema kuwa Chuo kIkuu Huria cha Tanzania kipekee kitamkumkumbuka na kumuenzi muasisi huyo kwa juhudi na maono ya uanzishawaji wake kwani aliamini kuwa elimu haina mwisho na kwamba watanzania wengi wangeweza kupata elimu kupitia mfumo usio rasmi kupitia chuo hicho.

Alisema  elimu ndio msingi wa taifa lolote na kwamba kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania watanzania wanaweza kupata elimu ambayo itawasaidia kwenda sambamba na mahitaji katika soko la ajira kwa kusisitiza masuala ya kujiajiri katika sekta isiyo rasmi ikiwemo ujasiriamali wakati taifa likielekea kwenye uchumi wa kati.

Kwa upande wake, Dkt Lawi Yohana, ambaye alimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma chuoni hapo alisema kuwa kuwa muhadhara huo ni sehemu ya elimu kwa jamii na utekelezaji wa majukumu ya chuo kikuu chochote amabayo ni ufundishaji, ushauri wa kitaalamu na kufanya tafiti.

Dkt Lawi alisema kuwa mhadhara huo ni mwanzo mzuri wa kuendelea kuenzi fikra za Mwl Nyerere huku tukijiuliza rasilimali tulizonazo na matumizi yake yanaendana vipi na falsafa za muasisi huyo.

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano chuoni hapo, Bi Kahenga Dachi alisema kuwa lengo la mhadhara huo ni kuenzi yale yote ambayo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyapigania kwa manufaa ya nchi  na bara la Afrika kwa ujumla.

Mhadhara huo umeratibiwa na Kurugenzi ya Masoko na Mawasiliano chuoni hapo na mada kuu ikiwa ni
“Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Chuo Kikuu Huria, Ujasiriamali na Uchumi wa Viwanda”.

No comments: