Thursday 20 October 2016



Serikali kuhamasisha wananchi kuuelewa mpango wa kuondoa ukatili kwa wanawake na watoto
Na Vincent Mpepo-OUT
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa ndani na nje imekusudia kuanza utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano wenye lengo la kumaliza kabisa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Sihaba Nkinga wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa kumaliza ukatili kwa wanawake na watoto iliyofanyika jijini Dar es salaam.
Bi alisema kuwa serikali imekusudia kushirikisha waizara na idara mbalimbali katika utekelezaji wa mpango huo ili kujenga dhana ya upamoja na kuifikia Jamii kwa haraka hivyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu masuala ya haki za wanawake na watoto.
“Uhamasishaji kwa jamii kuuelewa mpango kazi huu ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo tunapaswa kushirirkiana ili kufanikisha adhma hii ya kuwakomboa Wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi yao”, alisema Bi Nkinga
Alisema kuwa serikali imejidhatiti kushirikiana na wadau wa maendeleo kufanikisha mpango huo ili kulinda hadhi tulipewa kama nchi kwa kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee kwa Afrika amabayo imeonesha utekelezaji kwa vitendo ijapokuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kufikia malengo.
Aidha alisema kuwa uhamasishaji na utekelezaji wa mpango kazi huo utahusisha asasi za kiraia na taasisi mabalimbali sizizo za kiserikali na dini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto, Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Maragareth Mussai alisema kuwa mpango kazi huo umezingatia masuala mtambuka ikiwemo utengaji wa bajeti kwa makundi mbalimbali yanayojishughulisha na Wanawake na watoto.
“Bajeti imewekwa katika ngazi zote ili kurahisisha utekelezaji wa mpango kazi huu ikiwemo uwezeshaji kwa wafanyakazi katika idara mbalimbali katika ununuzi wa vifaa, vyombo vya usafiri na vitendea kazi”, alisema Bi Mussai.
Naye pedro Guerra, Mtaalamu wa Masuala ya Haki za watoto alisema kuwa watoto ni waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili hivyo huathirika kisaikolojia na makuzi ya ubongo wao.
“Matokeo ya tafiti tulizofanya yananoessha watato wa Tanzania wanakabiliwa na msongo wa mawazo katika ngazi ya familia, mazingira ya shule na wanaowafanyia ukatili huo ni ndugu wa karibu”, alisema Guerra. 
Madhumuni ya mafunzo hayo ya siku moja yalikuwa ni kuwafundisha waandishi wa habari namna ya kuripoti habari mbalimbalimbali kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na Wanawake Tanzania.

No comments: