Saturday 27 August 2016



Serikali yashauriwa kuboresha sera ya uchumi
Na Vincent Mpepo-OUT
Serikali imeshauriwa kuboresha sera na mifumo ya uchumi wa viwanda ambayo itasaidia kuleta maendeleo ya haraka katika kukabiliana na umasikini na kuboresha hali za maisha ya watanzania hivyo kukuza uchumi wa nchi na pato la mtu mmoja mmoja.
Ushauri huo ulitolewa na wahiriki wa warsha ya Sera za Viwanda, Mifumo ya Uchumi  na Mabadiliko ya Kimaendeo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es Salaam.
Mtoa mada katika warsha hiyo, Dk Piergiuseppe Fortunato  alisema kuwa nchi za Afrika zinatakiwa kutunga sera mathubuti za uchumi   wa viwanda  zitakazosaidia kutatua changamoto za umaskini, ukosefu wa ajira na teknolojia duni.
Maendeleo ya kiuchumi katika nchi yoyote yanaenda sanjali na uwepo wa sera na mifumo madhubuti ya itakayosimamia matumizi bora ya rasirimali na  kutatua changamoto zinazoikabili nchi, alisema Dk Fortunato.
Alisema serikali za nchi za Afrika zinahitaji sera ambazo zitagusa sekta maalumu  kwa nchi husika na mifumo ya uzalishaji katika sekta hizo ili kuzipa msukumo utakaoleta matokeo mazuri na tija katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akichangia mada katika warsha hiyo, Sylivatus Kashaga kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi alisema kuwa warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa imemsaidia kujifunza uzoefu kutoka nchi zilizofanya vizuri kwa mfano Vietnam ambayo uchumi wake kwa sasa umeimarika.
Kwa kuangalia takwimu inaonesha kuwa Tanzania na Vietnam tulianza pamoja kwa kuwa malengo ya kilimo na mazingira yanafanana likini wao wamepiga hatua zaidi ndio maana kuna wakati tumekuwa tunaagiza mchele kutoka Vietnam,alisema Kashaga.
Aliongeza kuwa bado kuna nafasi ya Tanzania kufanya vizuri katika uchumi kwa kuwekeza katika kilimo na uzalishaji wa mazao ya biashara kwa kuyaongezea thamani hivyo kukuza masoko ya kitaifa na kimaifa.
Dk Deusdedit Rwehumbiza kutoka Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa warsha hiyo imesaidia washiriki kujadili na kuainisha maeneo katika uzalishaji wa viwanda ambayo yanaweza kuikomboa nchi kiuchumi iwapo yatapewa kipaumbele.

Pia alisema,” warsha hiyo imekuja wakati muafaka wakati Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika juhudi za kufufua na kuanzisha viwanda vipya kama mkakati wenye lengo la kuimboa nchi kiuchumi.
Kwa upande wake, Akinyi Sassi, Mhadhiri Msaidizi katika Kitivo cha Uongozi wa Biashara-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alisema kuwa warsha hiyo imewasaidia kuwakumbusha washiriki matumizi mazuri ya rasilimali za nchi kwa kuangalia manufaa ya muda mrefu kuliko ya muda mfupi.
Akitolea mfano ugunduzi wa gesi Sassi alisema kuwa ni vizuri kwa nchi kujenga uwezo kwa Watanzania kuvuna na kuzitumia maliasili za nchi kwa manufaa yao kuliko kuwa na uwekekezaji ambao utadumu kwa muda mfupi na kufifia hapo baadaye.
Tunakaribisha wawekezaji kutoka nje, lakini tunatakiwa kuhakikisha kuwa Watanzania wanawekeza kwenye maeneo mengine, ili ikitotokea maliasili zetu zinapungua au kwisha tunabaki kwenye uchumi imara, alisema.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Taaluma), Profesa Muganda alisema kuwa washiriki watumie mafunzo na mijadala katika warsha hiyo  kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao na kuwaasa watunga sera kuchukua masuala muhimu yaliyojadiliwa na kuyafanyia kazi.
Warsha hiyo ya siku tatu iliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa lijulikanalo kama UNICTAD linaloshughulikia masuala ya biashara na maendeleo ya uchumi kwa kushirikiana na Kitivo cha Uongozi wa Biashara-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kuhudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka katika Taasisi za Elimu ya Juu, watunga sera na wawalikishi kutoka wizara mbalimbali.

No comments: