OUT yamkumbuka Mwl Nyerere
kwa Muhadhara
Na Vincent Mpepo-OUT
Katika kuadhimisha miaka 17 ya
kifo cha Baba wa Taifa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeadhimisha kwa kufanya
muhadhara wa wazi ambao umeshirikisha wanazuoni katika fani mbalimbali chuoni
hapo na mada kuu iliwasilishwa kama sehemu ya kukumbuka na kuenzi mchango wa
muasisi huyo kwa Taifa.
Akiwasilisha mada katika mhadhara
huo, Mhadhiri Mwandamizi Dkt Neville Reuben alisema kuwa Mwl Nyerere alikuwa na
maono ambayo kama yangeendelezwa kiutekelezaji yangesaidia kulifikisha taifa
hili mbali katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwani alisisitiza
katika elimu.
“Mwl Nyerere aliamini kuwa elimu
ndiyo nyenzo kuu ya kuondoa ujinga, umaskini na maradhi”, alisema Dkt. Reuben
Alisema kuwa Chuo kIkuu Huria cha
Tanzania kipekee kitamkumkumbuka na kumuenzi muasisi huyo kwa juhudi na maono
ya uanzishawaji wake kwani aliamini kuwa elimu haina mwisho na kwamba
watanzania wengi wangeweza kupata elimu kupitia mfumo usio rasmi kupitia chuo hicho.
Alisema elimu ndio msingi wa taifa lolote na kwamba
kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania watanzania wanaweza kupata elimu ambayo
itawasaidia kwenda sambamba na mahitaji katika soko la ajira kwa kusisitiza
masuala ya kujiajiri katika sekta isiyo rasmi ikiwemo ujasiriamali wakati taifa
likielekea kwenye uchumi wa kati.
Kwa upande wake, Dkt Lawi Yohana, ambaye alimuwakilisha
Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma chuoni hapo alisema kuwa kuwa muhadhara huo ni
sehemu ya elimu kwa jamii na utekelezaji wa majukumu ya chuo kikuu chochote amabayo
ni ufundishaji, ushauri wa kitaalamu na kufanya tafiti.
Dkt Lawi alisema kuwa mhadhara huo ni mwanzo mzuri wa
kuendelea kuenzi fikra za Mwl Nyerere huku tukijiuliza rasilimali tulizonazo na
matumizi yake yanaendana vipi na falsafa za muasisi huyo.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano chuoni hapo, Bi Kahenga Dachi
alisema kuwa lengo la mhadhara huo ni kuenzi yale yote ambayo Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere aliyapigania kwa manufaa ya nchi na bara la Afrika kwa ujumla.
Mhadhara huo umeratibiwa na Kurugenzi ya Masoko na
Mawasiliano chuoni hapo na mada kuu ikiwa ni
“Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Chuo Kikuu Huria,
Ujasiriamali na Uchumi wa Viwanda”.